SIMBA SC imesitisha mpango wa kuwasajili kiungo Mzambia, Jonas Sakuwaha na mshambuliaji na Antonio Dayo Domingues kutoka Msumbiji.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe leo akizungumza nasi mjini Dar es Salaam.
Poppe, Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema kwamba katika dirisha hili dogo Simba imeacha na kusajili mchezaji mmoja mmoja tu wa kigeni ili kuimarisha kikosi chake.
Amemtaja mchezaji aliyeachwa ni beki Mzimbabwe Method Mwanjali na kwamba anayesajiliwa ni Mghana, Asante Kwasi kutoka Lipuli ya Iringa. Aidha, Poppe amesema Jamal Mnyate amekwenda Lipuli kwa mkopo.
Awali kulikuwa kuna tetesi za Simba kuwaacha wachezaji watatu na kusajili watatu wapya wa kigeni – kwamba pamoja na Mwangali wangeachwa pia washambuliaji Mghana Nicholas Gyan na Mrundi Laudit Mavugo, ili pamoja na Kwasi wasajiliwe pia Sakuwaha na Dominguez.
Na Dominguez alionekana kwenye picha akiwa na Kaimu Rais wa Simba SC, Salim Abdallah ‘Again’ wakisaini mikataba.
Kuhusu Dominguez, Poppe amesemal; “Mipango haikukamilika,”.
Wakati huo huo: Beki wa kati wa Simba, Salim Mbonde anatarajiwa kuanza mazoezi Jumatatu baada ya kupona maumivu ya goti yaliyomuweka nje tangu Oktoba 15, mwaka huu alipoumia kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Uhuru.
Daktari wa Simba SC, Yassin Gembe ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online kwamba Mbonde ataanza mazoezi mepesi Jumatatu baada ya vipimo kuthibitisha amepona.
Aidha, Gembe amesema kwamba kipa Said Mohammed Ndunda ambaye kwa pamoja na Mbonde wamesajiliwa kutoka Mtibwa Sugar msimu huu, naye anaingia katika wiki ya pili tangu aanze mazoezi ya gym. Majeruhi wengine, Emmanuel Okwi na Shomary Kapombe wanaendelea na matibabu.
Tupe Maoni Yako