Thursday, December 7, 2017

Mawingu Tz

Mo Dewji Aahidi Kutorudia Makosa Ya Mwaka 1993



AMA kweli Mohamed Dewji ‘Mo’ anaipenda mno Simba, kwani wakati baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo wakiwa wameshasahau kilichoitokea timu yao mwaka 1993, mfanyabiashara huyo bado anakumbuka na sasa ameweka wazi kuwa hawatarudia makosa waliyoyafanya mwaka huo.
Iko hivi! Mwaka huo Simba ilifanikiwa kutinga fainali michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika wakati huo likijulikana kama Kombe la Caf, lakini wakafungwa kizembe na Stella Abidjan ya Ivory Coast tena kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), Dar es Salaam.
Katika mchezo wa kwanza, Simba wakiwa ugenini walipambana vilivyo na kufanikiwa kupata suluhu, lakini wakajikuta wakifungwa mabao 2-0 kwenye uwanja wao wa nyumbani na kuwafanya mashabiki wao kurudi nyumbani vichwa chini.
Simba ndiyo timu pekee nchini kujitutumua na kufika hatua hiyo ambapo wakati kila mmoja akiamini watamaliza mchezo mapema nyumbani baada ya kupata suluhu ugenini, ghafla wakafungwa mabao hayo 2-0 kitu ambacho kinautesa moyo wa Mo Dewji, mpaka leo.
Tayari Mo ameshatangaza kutoa donge nono la usajili baada ya mwishoni mwa wiki hii wanachama wa Simba kwa kauli moja kukubali kumpa timu awekeze hisa za 49%, huku mfanyabiashara huyo hasira zake zikiwa ni kuona timu yao ikitwaa makombe makubwa Afrika.
Kigogo mmoja wa Simba ambaye ni rafiki wa karibu wa ‘Mo’, ameliambia BINGWA kuwa bilionea huyo amekumbushia jinsi anavyoumia roho akiukumbuka mchezo huo dhidi ya Stella na sasa anataka kufanya kitu ambacho kitawafurahisha mashabiki wao.
“Ule mchezo Simba walioshindwa kutwaa ubingwa dhidi ya Stella Abidjan, bado jamaa (Mo Dewji), anaukumbuka na anasema anakereka sana jinsi mashabiki walivyomiminika uwanjani wakaondoka wakiwa wanyonge.
“Lakini pia kama unakumbuka Simba wanayo misimu kama mitano hivi tunashindwa kushiriki michuano ya kimataifa, kitu ambacho Mo anaona ni kama kushushwa hadhi kwa jina la klabu yetu ndiyo maana ukaona anatoa ahadi za kufanya usajili wa nguvu.
“Kilichopo tuzidi kuomba Mungu atupe uhai maana kama hayo aliyoyaweka kwenye mipango yake yatakwenda vizuri, bila shaka tutakuwa tukipambana na timu kubwa kama TP Mazembe, Al Ahly na nyingine kuliko sasa ambapo eti timu kama Lipuli inaweza kutusumbua,” alisema kigogo huyo.
mwisho
-Bingwa

Tupe Maoni Yako