Thursday, December 7, 2017

Mawingu Tz

Samatta Aeleza Anavyomfahamu Straika Mzambia Anaekaribia Kusajiliwa Simba

STRAIKA wa KRC Genk ya Ubelgiji na nahodha wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta ameeleza jinsi anavyomfahamu straika wa Zesco Jonas Sakuhawa anayeendelea na majaribio katika klabu ya Simba.
Samatta alicheza na straika huyo kwa zaidi ya misimu miwili kwenye klabu ya TP Mazembe hivyo ni mtu anayefahamu vizuri uwezo wake.
Akizungumza nasi  akiwa nchini Ubelgiji anakoendelea kuuguza majeraha yake ya goti alilofanyiwa upasuaji, Samatta alisema mshambuliaji huyo ana sifa kubwa mbili ambazo zinaweza kuisaidia Simba kama atawashawishi kwenye majaribio yake.
“Namfahamu vizuri, alisajiliwa Mazembe akanikuta ingawa baada ya misimu miwili alipelekwa kwa mkopo kwenye klabu moja nchini kwao kisha akarejea tena na kupelekwa Don Bosco.
“Kama atawashawishi Simba wakamsajili anaweza kuwasaidia kutokana na mambo mawili ambayo ni tabia yake ya upambanaji uwanjani na uzoefu alionao, amecheza muda mrefu karibu na lango, hivyo si mtu wa kubabaika tena,” alisema Samatta.

Sakuhawa akiwa anaitumikia timu ya taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’
Sakuhawa 34, ambaye alikuwa akiwekwa benchi na Samatta kwenye kikosi cha Mazembe aliamua kurejea nchini kwao Zambia na kujiunga na Zesco mara baada ya kumaliza mkataba wake.

“Mimi na yeye tulikuwa tunacheza nafasi moja, mara nyingi alikuwa akiingia pale mimi ninapopumzishwa ingawa katika mechi ambazo kocha alikuwa akihitaji tushambulie zaidi alikuwa akitupanga kwa pamoja,” alieleza Samatta.
Simba wamempa Sakuhawa siku saba za majaribio chini ya kocha msaidizi Masoud Djuma huku leo hii ikiwa ni siku yake ya nne. Kama atamshawishi kocha huyo anaweza kupewa mkataba ili kuchukua nafasi ya mchezaji mmoja wa kigeni, Laudit Mavugo akitajwa zaidi. 

Tupe Maoni Yako