Mchezaji wa Zanzibar Heroes Ibrahim Ahmada aliyepeleka kilio Kilimanjaro Stars anataka kuitwa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ baada ya kufanikiwa kupachika bao.
Ahmada ambaye alifunga goli la pili kwenye mchezo ambao Zanzibar Heroes wameshinda 2-1 dhidi ya Kilimanjaro Stars kwenye mashindano ya kombe la Chalenji nchini Kenya.
“Natamani kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ndio maana nimepambana kufunga kwenye mchezo wetu na Tanzania bara ili nionekane. Nimefurahi sana timu kuipa ushindi timu yangu,” amesema Ahmada wakati akihojiwa na Azam TV.
Nyota huyo anaecheza ligi kuu ya Zanzibar amesema, walipoingia kwenye vyumba vya kubadilishia kocha Morocco aliwaambia wanatakiwa kutulia kwa sababu bado wananafasi ya kushinda mchezo.
“Tulipoingia kwenye vyumba vya kubadilishia, kocha alituambia tuwe watulivu kipindi cha pili tunaweza kusawazisha na kufunga magoli zaidi ya mawili. Tulimwamini kocha na sisi tukajiamini ndio maana tumepata matokeo haya.”
Katika mchezo huo Kilimanjaro ilianza kufunga goli dakika ya 29 kupitia kwa Himid Mao (nahodha) lakini Zanzibar Heroes walisawazisha dakika ya 66 goli likifungwa na Kassim Khamisi huku Ibrahim Ahmada akiua mechi kwa kuunga goli la ushindi kwa Heroes dakika ya 78.
- Zanzibar Heroes imeshinda mechi mbili kwenye kundi lake (Kundi A) mchezo wao wa kwanza walishinda 3-1 dhidi ya Rwanda kisha wameshinda leo 2-1 dhidi ya Kilimanjaro Stars.
- Watoto hao wa visiwani wamefikisha pointi 6 huku wakiwa wamefunga magoli matano na wenyewe wameruhusu magoli mawili.
- Kassim Khamis baada ya kufunga dhidi ya Kili Stars, amefikisha magoli mawili kwenye michuano ya Challenge Cup 2017. Goli lake la kwanza alifunga dhidi ya Rwanda Zanzibar Heroes iliposhinda 3-1.
- Kilimanjaro Stars haijashinda mchezo kati ya mechi mbili walizocheza (Libya 0-0 Kilimanjaro Stars, Kilimanjaro Stars 1-2 Zanzibar Heroes) imefungwa magoli mawili, imefunga goli moja.
Tupe Maoni Yako