Thursday, December 21, 2017

Mawingu Tz

Lwandamina Ailia "Chabo" Shelisheli Kuelekea Michuano Ya Klabu Bingwa Afrika


PAMOJA na uwepo wa ratiba za michuano ya Kombe la FA, Kombe la mapinduzi na Ligi Kuu bara, kocha wa Yanga, George Lwandamina ameanza kuifuatilia klabu ya St. Lois ya Shelisheli ambayo watakumbana nayo katika mzunguuko wa kwanza Klabu Bingwa Afrika.

Lwandamina amesema kwamba klabu ya St Lois imefanya mabadiliko makubwa ya kiufundi na hawataingia uwanjani kwa kuidharau hata kidogo.

“Nimetumia muda mwingi kuifuatilia, sio timu nyepesi kama ambavyo watu wanazungumza hivyo tunalazimika kuingia uwanjani kwa kutoidharau kama tunataka kusogea mbele,” alisema Lwandamina.


“Wamewekeza vizuri katika kikosi chao, hatutawadharau hata kidogo, kuna mapinduzi makubwa kwenye soka katika miaka ya hivi karibuni, hakuna timu ndogo wala kubwa. Ukizembea timu yoyote itakuadhibu,” aliongeza.

“Lengo letu ni kuvuka hatua tuliyoishia msimu uliopita na kwa kuanza lazima tuonyeshe hilo kuanzia mechi ya kwanza bila kujali tunakutana na timu kutoka ukanda upi.”

Katika droo iliyofanyika makao makuu ya Shirikisho la soka Afrika (CAF), timu 59 zimepangwa katika Ligi ya mabingwa na 44 zimo katika Kombe la Shirikisho.


Yanga ikivuka hatua hii itakutana na mshindi kati ya Township Rollers ya Botswana na El Merreikh ya Sudan.



Tupe Maoni Yako