AKIICHEZEA kwa mara ya kwanza timu yake mpya ya Yanga, mshambuliaji mpya, Yohana Nkomola, amethibitisha ubora wake baada ya kuonyesha kiwango kikubwa ndani ya dakika 20 tu. Nkomola aliyeng’ara akiwa na kikosi cha Serengeti Boys kilichoshiriki michuano ya Afcon ya vijana Mei, mwaka huu, amesaini mkataba wa kuichezea Yanga hivi karibuni katika usajili wa dirisha dogo.
Mshambuliaji huyo alijiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili sambamba na beki kutoka DR Congo, Fiston Kayembe. Nyota huyo, wikiendi iliyopita aliicheza Yanga mechi hiyo ya kirafiki dhidi ya Polisi Tanzania, mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru na matokeo kumalizika kwa suluhu.
Katika mechi hiyo, mshambuliaji huyo aliingia uwanjani na kuonyesha cheche zake katika dakika 70 ya mchezo huo akichukua nafasi ya Emmanuel Martin. Mshambuliaji huyo, mara baada ya kuingia, alibadilisha mchezo pamoja na kiungo mkabaji, Papy Kabamba Tshishimbi walioingia pamoja.
Nkomola aliwathibitishia ubora wake mashabiki waliojitokeza kuwatazama wachezaji waliosajiliwa na timu hiyo akitumia muda huo kupiga mashuti matatu. Mawili kati ya hayo yalipanguliwa huku moja likitoka nje. Mbali na mashuti hayo, dogo huyo alitengeneza nafasi mbili ambazo zote hazikuzaa matunda baada ya mshambuliaji Amissi Tambwe na Burhani Akilimali kushindwa kuzitumia vyema.
Nkomola aliendelea kuthibitisha ubora wake kwa kontroo safi, upigaji wa pasi safi zilizonyooka huku akipoteza pasi moja kwa muda wote aliokuwepo uwanjani. Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alisifia kiwango cha mshambuliaji huyo akiwaomba mashabiki wa timu hiyo kumpa ushirikiano.
“Ni mwanzo mzuri wa Nkomola kwani amejitahidi kucheza vizuri bila ya presha yoyote tofauti na wachezaji wengine wapya wanaokuja kuichezea Yanga,” alisema Cannavaro.
Tupe Maoni Yako