Tuesday, December 12, 2017

Mawingu Tz

Kichuya Aitega Simba Mkataba Mpya


WINGA wa timu ya Simba, Shiza Kichuya, amesema hatakuwa tayari kusaini kandarasi mpya ya kuendelea kukipiga kwa Wekundu hao wa Msimbazi kama hakutakuwa na maboresho ya mkataba.
Uongozi wa Simba unasubiri michuano ya Chalenji inayofanyika nchini Kenya imalizike ili kumalizana na Kichuya ambaye amebakiza miezi mitano katika mkataba wa miaka miwili aliosaini awali.
Kichuya alijiunga na Simba akitokea klabu ya Mtibwa Sugar, ambapo tangu atue kwa Wekundu hao Msimbazi, amekuwa ni msaada mkubwa kutokana na kuifungia timu yake mabao 12 kati ya 50 yaliyofungwa msimu uliopita.
Pia amekuwa akiipatia timu yake ushindi katika michezo muhimu hususani wanapokutana na mahasimu wao Yanga pamoja na Azam FC.
Akizungumza na Chandimu  kwa njia ya mtandao akiwa nchini Kenya ambako anaitumikia timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ katika michuano ya Chalenji, Kichuya alisema amezungumza na meneja wake juu ya kukaa mezani na Simba ili kuangalia namna ya kuboresha mkataba.
“Nipo tayari kuendelea kuitumikia Simba kwa misimu mingine miwili nikimaliza mkataba wa sasa, lakini ni lazima tuangalie mambo ya kuboresha na pia kipengele cha kucheza soka la kulipwa kipewe nafasi,” alisema.
Alisema kwa sasa hafikirii kucheza soka hapa nchini pekee, hivyo mkataba mpya ni muhimu ukazingatia kipengele kinachohusu soka la kulipwa.
“Pia mshahara na fedha za kusaini mkataba ni vitu muhimu kwangu, sitaki kufanya mzaha kwa kuwa hii ni ajira inayoendesha maisha yangu na familia,” alisema Kichuya.

Tupe Maoni Yako