Friday, December 22, 2017

Mawingu Tz

Yanga ‘Full’ Shangwe, Wachezaji, Benchi La Ufundi, Mashabiki Meno Nje


KIUNGO wa Kimataifa wa Yanga, Mzimbabwe Thaban Kamusoko, amerejea uwanjani jana na kuwashtua baadhi ya mashabiki waliofika kuangalia mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kurejea kwa Kamusoko kikosini kumeamsha shangwe miongoni mwa wachezaji, benchi la ufundi na hata mashabiki wa Yanga, wakiamini ‘chama’ litakuwa limekamilika tayari kuuwasha moto katika mechi zao zijazo za Ligi Kuu Tanzania Bara na hatimaye kutetea ubingwa wao.
Ikumbukwe Yanga imeshindwa kufanya usajili wa wachezaji nyota iliyokuwa ikiwapigia hesabu kutokana na ukata, huku watani wao wa jadi, Simba, wakifanikiwa kufanya hivyo, wakiwa wamewanasa wakali watatu wa kigeni; Jonas Sekuwaha, Antonio Domingos (Msumbiji) na Asante Kwasi (Ghana), ambaye hata hivyo, usajili wake kutoka Lipuli umezua utata.
Japo Yanga hawajafanya usajili wa maana zaidi ya kumnasa kinda wa Serengeti Boys, Yohana Mkomola na beki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Fiston Kayembe, lakini wamekuwa wakijipa matumaini ya kufanya vema na hatimaye kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Bara, inayodhaminiwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania.

Tupe Maoni Yako