MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, wameanza mazoezi leo Jumatatu lakini mlinda mlango wao, Beno Kakolanya amegoma kwenda mpaka alipwe pesa zake za usajili.
Kakolanya ambaye hivi karibuni meneja wake, Seleman Haroub aliweka wazi madai yao hadharani kuwa Yanga yenye maskani yake Jangwani, haijamlipa kipa huyo pesa zake za usajili.
Sasa sakata hilo limefikia patamu, Yanga wamekaa kimya na Kakolanya pia, lakini habari za ndani ni kwamba, Haroub yupo Dar es Salaam na leo Jumatatu upo uwezekano ukimya huo ukavunjika endapo pande hizo mbili zitakaa pamoja na kutatua suala hilo.
"Kama Yanga watashindwa kulipa pesa hizo, moja kwa moja mkataba huo utakuwa kama umevunjika na Kakolanya atakuwa huru kwenda timu yoyote katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili, lakini mazunguko ya leo ndiyo yatatoa majibu kamili,"anasema mtu wa karibu wa Kakolanya.
Hata hivyo, Yanga hawakuweza kupatikana kwa ajili ya kutolea ufafanuzi suala hili, simu ya Katibu Mkuu Charles Mkwasa iliita bila mafanikio.
Tupe Maoni Yako