Tuesday, December 5, 2017

Mawingu Tz

Ngoma Amerejea Na Ripoti Mkononi, Mkwasa Ametoa Msimamo Wa Yanga

Mshambuliaji wa Yanga amesharejea nchini akitokea nchini kwao Zimbabwe na kwenda kuripoti kwa uongozi wa klabu hiyo huku akiwa na ripoti ya mtaalam wake wa viungo inayodai anatakiwa aendelee kupumzika kwa muda wa wiki sita.
Katibu mkuu wa Yanga Charles Boniface Mkwasa amethibitisha kurejea kwa mshambuliaji ambaye aliondoka bila kutoa taarifa ndani ya klabu, lakini Mkwasa amesema kwamba, maelezo na ripoti aliyokuja nayo Ngoma bado hayajitoshelezi.
“Bado maelezo hayajitoshelezi kwa maana ya kwamba, ripoti imeandikwa na physiotherapist wake lakini baada ya kutafakari tunahitaji tupate ripoti kamili kutoka kwa daktari ambaye ndio anaweza kutoa tamko lakini nafikiri kama yeye hatuja kaa kuongea zaidi lakini cha msingi amesharejea na ameripoti.”
“Anadai alikuwa kwenye matibabu Zimbabwe, sisi tunataka maelezo ya daktari aliyekuwa akimtibia, tumemuuliza alikuwa wapi akatueleza alikuwa anatibiwa sasa tunahitaji taarifa ya daktari inayoonesha magonjwa yaliyokuwa yakimsibu.”
Licha ya kwamba Ngoma alikuwa anatibiwa nchini kwao, ripoti aliyoiwasilisha Yanga inaonesha bado anatakiwa kuendelea kupumzika.
“Pamoja na kudai alikuwa anatibiwa lakini kuna ripoti inaeleza anatakiwa akae wiki sita (6), sasa hata haijitoshelezi vizuri, tunataka taarifa rasmi kutoka kwa daktari wake ambayo inaweza kueleza vizuri zaidi kama anapumzika kwa muda gani na lini atakuwa tayari atakapohitajika.”
Baada ya Ngoma kurejea huku sababu kubwa ya kuondoka bila kuaga ikiwa ni kwenda kutibiwa nchini kwao, Mkwasa ametoa msimamo wa Yanga kuhusu nini kitafanyika.
“Ni kufuata taratibu, kwa mujibu wa taratibu zetu ni kwamba, lazima tupate taarifa kutoka kwa daktari aliyekuwa akimtibu sasa hapa amekuja na ripoti ya daktari wa viungo kwa hiyo kinachotakiwa tunataka tupate ripoti ya daktari kwa hiyo tunataka tumuone Ngoma tumueleze.”
Endapo ikigundulika ni kweli Ngoma alikuwa anatibiwa na anatakiwa kupumzika kwa muda huo uliotajwa, itampunguzia adhabu kutoka kwa uongozi wake?
“Hilo ni suala linguine na suala la matibabu ni lingine, kwa hiyo sisi tutafuata taratibu zetu za kazi na taratibu za mikataba ziko wazi na hazitaki kujieleza, kama mtu amechelewa kuripoti kuna taratibu zinachukuliwa au kama kuna kosa linafanyika kila kitu kinajitosheleza zenyewe.”
Klabu ya Yanga itaendelea kumtibu Ngoma kutoka pale ambapo daktari wake ameishia ili kuona namna gani wanamsaidia mchezaji? Mkwasa amefafanua.
“Sisi tunahitaji huduma ya mchezaji kwa sababu amepewa kandarasi ya kuitumikia klabu kwa hiyo klabu inategemea yeye aitumikie na siyo yeye tu hata mchezaji mwingine ambaye ana majeruhi kwa hiyo klabu inaingia gharama za kumtafutia vibali na kumlipa ili afanye kazi sasa kama kuna kuwa kuna upande mmoja unaumia halafu upane mwingine hauathiriki basi lazima tuangalie kitu gani cha kufanya.”
-Shaffih dauda

Tupe Maoni Yako