Friday, December 22, 2017

Mawingu Tz

Man U, Man City, Chelsea, Liver Zikiwasajili Mastaa Hawa Januari Itapendeza Zaidi



ZIMEBAKI siku chache kabla ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa nchini England.
Wakati zikiwa zimeshabaki siku hizo chache, tayari kuna baadhi ya makocha ambao wameshatangaza kuingia sokoni ili kujaza nafasi ambazo zimeonekana kuwa na upungufu katika raundi hii ya kwanza na huku wengine wakieleza kuwa itakuwa ni kama kupoteza muda.
Wanaosema ni kama kupoteza muda ni pamoja na Arsene Wenger wa Arsenal, lakini mwenzake Jose Mourinho akionekana kulisubiria kwa hamu dirisha hilo la majira ya joto.
Pamoja na Wenger kutoa madai hayo lakini alishawahi kuwasajili nyota kadhaa kama vile Andrey Arshavin, Nacho Monreal, Theo Walcott na Mohamed Elneny.
Licha ya wawili hao kuwa na mawazo tofauti, wachambuzi wa masuala ya soka wamejaribu kuangalia ni wachezaji wapi wanaweza kuzisaidia timu kubwa tano endapo watafanikiwa kunasa saini zao katika dirisha hilo dogo litakapofunguliwa na ifuatayo ni orodha hiyo:-
  1. Arsenal: Julian Draxler
Wakati mpaka sasa suala la nyota wake wawili Alexis Sanchez na Mesut Ozil kuhusu mikataba yao bado halijapatiwa ufumbuzi, kocha Arsene Wenger na klabu yake ya Arsenal wanakabiliwa na tatizo la kusaka mbadala wao.
Ili waweze kulimaliza, kiungo wa Paris Saint-Germain, Julian Draxler ambaye wamekuwa wakimwinda kwa misimu kadhaa, sasa ni wakati mwafaka kwao kuongeza kasi ili aweze kuokoa jahazi endapo nyota hao wawili wataendelea kuweka ngumu kusaini mikataba mpya.
Tofauti na ugumu uliokuwapo siku za nyuma, lakini sasa Arsenal wanaweza kupata mteremko kutokana na usajili ambao PSG waliufanya majira haya ya joto ambao ulishusha vifaa kama Neymar da Silva na Kylian Mbappe ambao tayari wameshamfunika nyota huyo na hivyo endapo Arsenal wataongeza juhudi inaweza kuwa rahisi kwao wakamnasa.
  1. Chelsea: Lucas Moura
Baada ya kufanya vizuri msimu wake wa kwanza alipotua Chelsea, kocha Antonio Conte, kwa sasa anaandamwa na shutuma kutokana na timu hiyo kutokuwa na matokeo ya kuridhisha.
Shutuma hizo zinatokana na kuwa baada ya kumfukuza straika wake, Diego Costa na kubaki na mastaa Willian na Michy Batshuayi, jambo hilo halijamsaidia kitu. Kutokana na ujio wa dirisha hilo dogo la usajili, ni nafasi pekee kwa kocha huyo kuweza kutua mzigo huo wa lawama wa nyota wa zamani wa klabu hiyo, Frank Lampard, anaamini Muitaliano huyo atasajili wachezaji wenye ubora.
Pamoja na kwamba Chelsea imeshatumia kitita cha pauni milioni 70 kumsajili Alvaro Morata, lakini suala la kusajili straika linapaswa kupewa kipaumbele.
Kutokana na hali hiyo, straika ambaye anaweza kumsaidia kocha huyo ni Lucas Moura, ambaye msimu huu amecheza dakika chache akiwa na timu ya Paris Saint-Germain.
  1. Liverpool: Leon Goretzka
Huku wakati ikiwa imebaki miezi michache kabla ya mkataba wake na timu ya Schalke kumalizika, klabu kubwa za Ligi Kuu England zikiwamo Liverpool na Arsenal, zimeshaanza kuonesha nia ya kutaka kumsajili.
Hata hivyo, mpaka sasa hakuna klabu ambayo imeshaonesha nia ya dhati kusaka huduma ya staa huyo kama ilivyokwa Liverpool.
Wakati nyota wake, Emre Can na Philippe Coutinho, wanahusishwa kutaka kuondoka jambo la kumsajili kiungo huyo Mjerumani Reds wanatakiwa kuelekeza jitihada zao kwa nyota huyo.
Pia kutokana na kwamba Schalke imeshapoteza wachezaji wengi wakiondoka wakiwa huru, hawataweza kukataa kitita cha pauni milioni 30 ili kumzuia mchezaji huyo ambaye ameshaonesha dhamira ya kweli ya msimu ujao kutotaka kuvaa tena uzi wa klabu hiyo ya Ligi ya Bundesliga.
  1. Manchester City: Inigo Martinez
Licha ya kuwa msimu huu Man City kuonekana kuwa vizuri, lakini bado inaonekana kuwa na upungufu kwenye safu yake ya kiungo wa kati na hivyo ili iweze kutwaa ubingwa, inalazimika kulimaliza tatizo hilo kwa haraka.
Hii ni kutokana na kwamba pamoja na kuwa na wastani wa mabao 3.2 kwa kila mechi na safu ya mabeki wa nyuma kuwa imara, lakini haiwezi kulinganishwa na Manchester United kwa kukaba kuanzia katikati.
Tatizo hilo lilianza kuonekana baada ya kuumia wachezaji wake, Benjamin Mendy na John Stones ambapo Eliaquim Mangala na Vincent Kompany, wanashindwa kuziba vyema nafasi zao na hivyo ili waweze kuondokana nalo, itabidi Januari wajitose sokoni ili kusaka beki wa kati mwingine na si mwingine bali ni Mhispania, Inigo Martinez.
  1. Manchester United: Willian
Manchester United mara zote huwa hawataki utani wakati linapofika suala la usajili.
Hii ni kutokana na kwamba mashetani hao wekundu wameshawahi kuwaliza mahasimu wao kwa usajili wa nyota kama vile Robin van Persie, Juan Mata na Nemanja Matic katika miaka ya hivi karibuni.
Kwa mara nyingine tena Manchester United inatajwa kumwinda winga wa Chelsea, Willian ambaye ameshatwaa ubingwa wa Ligi Kuu England mara mbili.
Mashetani hao wekundu wanaweza kunasa saini ya staa huyo kutokana na kwamba, kwa sasa hana maelewano mazuri na kocha wake, Antonio Conte na hivyo Man Utd wanatakiwa kuachana na mipango ya kuwafukuzia Ivan Perisic ama Gareth Bale ili kuweza kumwachia nafasi Mbrazili huyo atue Old Trafford.
Kutokana na ubora wake ikilinganishwa na chipukizi waliopo Marcus Rashford na Anthony Martial, anaweza kumsaidia Jose Mourinho kupigania ubingwa dhidi ya mahasimu wao katika Jiji la Manchesterna Man City.

Tupe Maoni Yako