Monday, January 8, 2018

Mawingu Tz

Tambwe Arejeshwa Dar Kwa Matibabu

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Mrundi Amissi Joselyn Tambwe amepanda boti mchana huu visiwani Zanzibar kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.
Daktari wa Yanga SC, Edward Bavu amesema leo kwamba Tambwe amelazimika kuondoka kambini mjini Zanzibar kurejea Dar es Salaam kwa  ajili ya matibabu zaidi ya Malaria.
“Ana Malaria, kwa siku zaidi ya nne sasa amekuwa na wakati mgumu, tumelazimika kumrejesha Dar es Salaam ili apatiwe matibabu zaidi,” amesema Dk. Bavu
Tambwe anaondoka wakati Yanga SC leo inateremka Uwanja wa Amaan, Zanzibar kumenyana na Singida United kuanzia Saa 2:15 usiku.Mrundi huyo amekuwa katika msimu mgumu, akianza kukaa nje tangu Agosti kutokana na maumivu ya goti kabla ya kurejea Desemba, lakini mapema Januari hii tena anaondolewa kambini kwa sababu ya Malaria.

Na hii inazidi kuipunguzia nguvu safu ya ushambuliaji ya Yanga kipindi hiki ambacho inawakosa wakali wake wengine wazoefu, Mzimbabwe Donald Ngoma na Mzambia, Obrey Chirwa. 
Yanga sasa itaendelea kumtegemea Ibrahim Ajib pekee katika washambuliaji wazoefu kwenye hatua iliyobaki ya Kombe la Mapinduzi – zaidi ya hapo ni chipukizi akina Yohanna Oscar Nkomola, Juma Mahadhi na Matheo Anthony.  


Tupe Maoni Yako