Tuesday, January 9, 2018

Mawingu Tz

Niyonzima Arejesha Matumaini Simba

WAKATI wenzake wakiwa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi huko visiwani Zanzibar, kiungo mchezeshaji wa Simba, Mnyar­wanda, Haruna Niyonzima yeye yupo jijini Dar es Salaam akiendelea kujifua ufukweni.
Mnyarwanda huyo alibaki Dar ku­tokana na majeraha ya enka anayoen­delea kuyauguza yaliyomuweka nje ya uwanja kwa muda wa wiki mbili.
Kiungo huyo, alipata majeraha hayo akiwa kwenye mazoezi ya timu hiyo wakati kikosi hicho kikiwa na Mcam­eroon, Joseph Omog aliyesitishiwa mkataba wake hivi karibuni kabla ya msaidizi wake Mrundi, Masoud Djuma kukabidhiwa.
Akizungumza na Championi Ju­matatu, Niyonzima alisema ameanza programu hiyo ya kukimbia ufukweni kwa ajili ya kuiponyesha enka hiyo ili ipone kabisa.
Niyonzima alisema, wakati akien­delea na matibabu mengine atafanya mazoezi ya ufukweni kwani mchanga ni sehemu ya tiba kwa ajili ya jeraha hilo la enka linalomsumbua.
Aliongeza kuwa, hataki kuona akiendelea kusumbuka na jeraha hilo ambalo mara kwa mara linamtokea ili atakaporejea uwanjani lisijirudie.
“Mimi nipo Dar na sipo na timu Zan­zibar, kama unavyofahamu bado enka inanisumbua na hivi sasa nipo nafanya mazoezi ya kukimbia ufukweni huku nikiendelea kupata matibabu mengine hospitali.
“Na mazoezi haya ya ufukweni nayo ni sehemu ya tiba kwangu, kwani mchanga nao ni tiba kwa jeraha hili la enka inayonisumbua kwa muda mrefu,” alisema Niyonzima aliyetua kuichezea Simba katika msimu huu.

Tupe Maoni Yako