Wednesday, December 27, 2017

Mawingu Tz

Himid Mao huyooo Yanga

SASA ni rasmi kuwa kiungo wa Azam, Himid Mao ‘Ninja’, anaweza kutua Yanga iliyokuwa ikimsaka kwa muda mrefu baada ya mchezaji huyo kushindwana na timu aliyokwenda kujiunga nayo ya Bidvest West ya Afrika Kusini.
Yanga ilikuwa ikimwania Mao tangu msimu uliopita, ikimwona kama suluhisho katika nafasi ya kiungo mkabaji.
Baada ya kumkosa, ilipiga hodi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kumtwaa Papy Tshishimbi aliyeonyesha kiwango cha hali ya juu na kuwa kipenzi cha mashabiki wa Wanajangwani hao.
Moja ya sababu iliyowafanya Yanga kumkosa Mao, ni mpango wa kiungo huyo kwenda kucheza soka la kulipwa Afrika Kusini.
Lakini habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana, zinasema kuwa Mao ameshindwana dau na Bidvest West na hivyo amerejea nchini kuendelea na maisha yake ndani ya Azam.
Kwa hali hiyo, iwapo Yanga wataendelea kumuhitaji, wanaweza kumtwaa mwishoni mwa msimu.
Chanzo cha kuaminika cha BINGWA kutoka ndani ya Azam, kinasema: “Kuna asilimia 75 za Himid Mao kubaki Azam kwani alipokwenda ‘South’ (Afrika Kusini) kwenye mazungumzo na klabu ya Bidvest, walishindwana katika suala la ‘mtonyo’ (fedha), hivyo msimu huu atabaki Azam, msimu ukimalizika anaweza kwenda timu nyingine lakini si Bidvest West tena.”
BINGWA lilimtafuta Mao kuzungumzia hilo ambapo alisema: “Nikweli nilikuwa Afrika Kusini, lakini siwezi kutaja ni klabu gani, pia sikuwa nimekwenda kwa lengo la kufanya majaribio kwani majaribio nilishafanya muda mrefu, nilienda kwa ajili ya mazungumzo na yamekwenda vizuri.”
Mao ni miongoni mwa viungo hodari wakabaji hapa nchini akiwa pia ni nahodha na tegemeo la timu ya Taifa, Taifa Stars.

Tupe Maoni Yako