Tuesday, December 26, 2017

Mawingu Tz

Hatima Ya Straika Wa Msumbiji Katika Kikosi Cha Simba Hii Hapa.

Klabu ya Simba imeamua kuachana na straika mkali wa kuchana nyavu kutoka Msumbiji, Dayo Antonio Domingos na badala yake kumbakisha kikosini Mrundi Laudit Mavungo.
Kwa wanaokumbuka mchana wa Ijumaa ya Desemba 15, straika huyo wa Ferroviario de Beira alitua nchini ikiwa ni saa chache kabla ya kufungwa kwa dirisha dogo la usajili kabla ya kuongezwa hadi Jumamosi iliyopita.
Straika huyo aliletwa ili kuchukua nafasi ya Mavugo aliyekuwa mbioni kutolewa kwa mkopo Arabuni, licha ya mwenyewe kung’ang’ania kutaka kwenda kucheza soka Kenya katika klabu ama Gor Mahia au AFC Leopards.
Mabosi wa Simba walimkimbiza mbiombio hotelini na kukaa naye faragha ili kumalizana naye kuwahi dirisha la usajili sawia na beki Mghana Asante Kwasi aliyechukuliwa kutoka Lipuli aliyetua Msimbazi kuziba nafasi ya Method Mwajali.
Asubuhi ya siku hiyo ikathibitika kuwa pande hizo mbili zimemalizana na hata picha zikasambazwa, lakini kumbe nyuma ya pazia, mipango ilikwama na ndio maana straika huyo aliamua kutimka kwao kimyakimya.
Ipo hivi. Simba imeshindwa kukamilisha usajili wa straika huyo iliyokuwa imempa mkataba wa miaka miwili baada ya kuchelewa kupata barua ya uhamisho kutoka kwao, hivyo kuamua kuachana naye rasmi.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba ni kwamba Domingos hatakuwa katika kikosi cha Simba labda mpaka msimu ujao kama wataendelea kumhitaji na badala yake Mavugo anabakishwa kikosini.
“Domingos alikuwa kwenye malengo yetu lakini vibali vyake havikukamilika ndiyo maana tulishindwa kuingiza jina lake kwenye usajili japo ni kweli tulimpa hata mkataba na aliusaini, ndiyo maana Mavugo yupo mpaka sasa, vinginevyo Mavugo tungemwachia ili aende alikotaka, “ alisema mmoja wa vigogo wa Simba aliyeomba kuhifadhiwa jina lake kwa vile hayupo Kamati ya Usajili.
Makamu Mwenyekiti wa Usajili Simba, Kassim Dewji alisema atakuwa na nafasi ya kuzungumzia usajili mzima wa Simba leo, hivyo kushindwa kuweka bayana juu ya Domingos kusepa Msimbazi.

Tupe Maoni Yako